Sunday, 24 May 2015

YANGA SC YA IZIDI UJANJA SIMBA SC


YANGA SC imewapiga bao wapinzani, Simba SC na Azam FC katika vita ya kuwania saini ya kiungo hodari wa pembeni, Deus Kaseke.
Kaseke amesaini Mkataba wa miaka miwili na Yanga SC asubuhi ya leo, makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam mbele ya Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Isaac Chanji.
Kaseke anatua Yanga SC kama mchezaji huru baada ya kumaliza Mkataba wake Mbeya City, aliyoichezea kwa miaka mine iliyopita.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya kusaini Mkataba huo, Kaseke amesema; “Nimefurahi kutua Yanga SC, ni timu ambayo kwa kweli nilikuwa nina ndoto za kuichezea kwa muda mrefu,”. 

Kaseke amesema anafahamu changamoto inayomkabili baada ya kusaini Yanga SC, ushindani wa nafasi dhidi ya wachezaji wengine bora waliopo kwa mabingwa hao wa Tanzania.
“Yanga SC ni timu kubwa, ina wachezaji bora na ndiyo maana ni mabingwa. Baada ya kusajili, sasa natakiwa kufanya mazoezi kwa bidii ili niwe katika kiwango bora zaidi na kuwashawishi makocha wanipe nafasi,”amesema.
Kaseke amesema lengo lake ni kufika mbali zaidi kisoka na anataka aitumie Yanga SC kama ngazi ya kupanda kwenda nje kucheza soka ya kulipwa.
Yanga SC wanamsajili Kaseke baada ya kumpoteza kiungo wake bora wa pembeni, aliyekuwa anaweza kucheza pia kama kiungo wa kati na mshambuliaji, Mrisho Ngassa aliyesaini Free State Stars ya Afrika Kusini.
Kaseke pia ana sifa kama Ngassa, mbali na kuteleza pembeni kwa kasi, pia anaweza kucheza kama kiungo wa kati na mshambuliaji.
Ilikuwa vita usiku wa kuamkia leo, viongozi wa Simba na Yanga wakifukuzana kumsaka Kaseke hadi hatimaye wana Jangwani kufanikiwa kumnasa na wamemalizana naye. 
Azam wenyewe walikuwa wanamfuatilia kimya kimya mchezaji huyo- na hawakuwa na spidi ambayo walikuwa nayo Simba SC- maana yake hili ni pigo zaidi kwa wana Msimbazi.

No comments:

Post a Comment