WAKATI Yanga SC wakisherehekea saini ya winga Deus Kaseke, Simba SC nao wamefanya yao mchana huu.
Kiungo hodari mchezeshaji Peter Mwalyanzi kutoka timu ile ile, Mbeya City aliyotokea Kaseke amesaini Mkataba wa miaka miwili kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.
Mwalyanzi moja ya viungo waliong’ara katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Barav msimu huu ambaye alikuwa anamchezesha vizuri Kaseke, amesaini ofisini kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe, Mbezi, Dar es Salaam.
Na Poppe aliyekuwa na Mjumbe wa Kamati ya Uteneaji, Collins Frisch akasema; “Sisi tunajua wachezaji bora na Simba SC ndiyo nyumbani kwa wachezaji bora,”.
Poppe amesema kwamba Mwalyanzi ni pendekezo la kocha Mserbia, Goran Kopunovic lakini hata washauri wengine wa masuala ya kitaalamu wameridhishwa na uwezo wa mchezaji huyo.
Kwa upande wake, Mwalyanzi ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba anajisikia furaha kusaini timu hiyo kubwa, kwani ni hatua moja kubwa mbele katika maisha yake ya soka.
“Mchezaji yeyote anapokuwa anaibuka katika nchi hii, ndoto zake ni siku moja kucheza timu kubwa kama hizi, na mimi nimefurahi sana kujiunga na Simba SC,”amesema.
Mwalyanzi ameongeza kwamba baada ya kusaini, anaomba ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzake, viongozi na mashabiki ili aweze kufanya vizuri.
Mapema leo, Yanga SC imemsainisha Mkataba wa miaka miwili kiungo mshambuliaji, Deus Kaseke makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam mbele ya Katibu Mkuu, Dk Jonas Tiboroha na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Isaac Chanji.
Kaseke anatua Yanga SC kama mchezaji huru baada ya kumaliza Mkataba wake Mbeya City, aliyoichezea kwa miaka mine iliyopita.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY baada ya kusaini Mkataba huo, Kaseke amesema; “Nimefurahi kutua Yanga SC, ni timu ambayo kwa kweli nilikuwa nina ndoto za kuichezea kwa muda mrefu,”.
Kaseke amesema anafahamu changamoto inayomkabili baada ya kusaini Yanga SC, ushindani wa nafasi dhidi ya wachezaji wengine bora waliopo kwa mabingwa hao wa Tanzania.
“Yanga SC ni timu kubwa, ina wachezaji bora na ndiyo maana ni mabingwa. Baada ya kusajili, sasa natakiwa kufanya mazoezi kwa bidii ili niwe katika kiwango bora zaidi na kuwashawishi makocha wanipe nafasi,”amesema.
No comments:
Post a Comment