Wednesday 26 August 2015

SIMBA SC YAFANIKIWA TENA

Mshambuliaji Pape Abdoulaye N'Daw mwenye umri wa miaka 21 anatarajiwa kutua leo usiku kutoka Dinamo Bucuresti ya Romania kufanya majaribio Simba SC 

SIMBA SC imeachana na Msenegali, Papa Niang baada ya kumjaribu kwa dakika 45 tu jana katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Mwadui FC ya Shinyanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hawajachoka, Simba SC leo wanatarajia kupokea wachezaji wawili wengine wa kigeni kuwafanyia majaribio, ambao ni Msenegali Pape Abdoulaye N'Daw na Mmali.
N'Daw mwenye umri wa miaka 21, kwa sasa anachezea klabu ya Liga I ya Romania, Dinamo București, wakati wa Mali bado jina lake halijapatikana na haijulikani anatoka timu gani. 
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia  CHENGULA NEWS leo kwamba wachezaji hao watafanyiwa majaribio na atakayevutia zaidi, ndiye atapewa Mkataba. 
Niang alikuja SImba SC baada ya klabu hiyo kushindwa kufikia makubaliano na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Kevin Ndayisenga juu ya dau la usajili.
Niang kutoka klabu ya Alianza F.C. ya El Salvador ambaye ni mdogo wa mshambuliaji wa kimataifa wa zamani wa Senegal, Mamadou Niang jana alishindwa kabisa kuwashawishi wana Simba kwa soka yake.

Mchezaji huyo wa zamani wa CF Mounana ya Gabon, Al Shabab SC ya Kuwait, FC Vostok ya Kazakhstan, FF Jaro, AC Oulu na FC OPA za Finland alitarajiwa kuondoka usiku wa jana kurejea kwao, ikiwa ni baada ya siku tatu za kuwa Dar es Salaam.
Awali Simba SC pi ilishindwa kumsajili mshambuliaji mwingine hatari wa Vital’O, Laudit Mavugo kufuatia klabu mbili za nchini humo kupandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 walizokubaliana awali.
Aidha, kuibuka pia kwa mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo na kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo nako kuliishitua Simba.
Vital’O ikaikoroga zaidi Simba SC baada ya kudai kiwepo kipengele cha wao kupata asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Wekundu hao wa Msimbazi kwenda klabu nyingine. 

No comments:

Post a Comment