Matatizo yanayochangia watu kuachana yako mengi, ambayo mtu unaweza
kujaza vitabu kuyaelezea, lakini uchunguzi unaonesha kuwa wapenzi
huachana kutokana na udhaifu wa sababu zilizowasababisha kupendana. Kwa
mfano wapenzi ambao wakati wa kupendana kwao walitamaniana kwa maumbo,
sura, mvuto wa kingono na pesa huwa katika hatari ya kuachana baada ya
vitu vilivyowasukuma kupendana kupoteza mvuto.
Hakuna asiyefahamu
kuwa watu hubadilika tabia, umbo, sura, hufirisika na hata kutovutia
tena! Hivyo mtu anapopenda kwa sababu hizo, ukomo wake huwa ni baada ya
alichopenda kuondoka. Ukipenda kwa tamaa ya ngono ukishashibishwa nayo
hutakuwa na sababu ya kumpenda mpenzi wako, matokeo yake utamwacha.
Ukiwa umeamua kumpenda dada fulani kwa sababu anavutia, kumbuka kuwa
anaweza kupata ajali akapoteza mvuto au akazeeka. Je umeshajiuliza swali
itakuwaje kama mpenzi wako atapata makovu, utafanyaje baada ya mvuto
wake wa usichana kuisha, nini kitafuata baada huyo mwanaume unayemsifia
kwa tendo la ndoa atakapofikia ukomo wa kukutosheleza? Nadhani ni
kuachana.
Sababu nyingine inayochangia wapenzi kuachana ni kutojali
changuo sahihi kulingana na jinsi mtu mwenyewe alivyo, (SOMA NJIA ZA
KUCHANGUA MCHUMBA KWENYE KITABU CHA TITANICNo 1).
Mimi niliwahi
kusoma katika Biblia Mungu akiweka wazi namna alivyozingatia kumuumbia
mke Adamu kwa kusema, alimuumba mtu wa kufanana naye. Hivyo ni busara
kupata mpenzi wa kufanana na wewe kwa tabia na mambo mengine ya msingi,
bila hivyo mapenzi hayawezi kudumu.
Kwa mfano kama wewe ni mtu wa
imani kali, inakuwaje unakwenda kupendana na mpagani, huoni hicho
kitakuwa kikwazo cha penzi lenu? Kwa msingi huo, lazima kupendana
kuambatane na kufanana elimu, mtazamo na hata tamaduni, hii itasaidia
kuondoa vikwazo vya mapenzi kuvunjika.
Lakini jambo jingine
linalowafanya wapenzi wengi kuachana ni kutojali au kutofahamu kanuni za
kutunza penzi. Kuna watu wanaweza kuchaguana kwa kuzingatia maelekezo
yote, lakini wakajikuta wanaachana kwa kutojua namna ya kukuza na
kudumisha upendo wao.
Nasema hivyo kwa sababu, kumpata mpenzi ni
jambo jingine na kumtunza ni hatua nyingine ambayo ni ya msingi.
Inawezekana kabisa ukampata wa kufanana naye, lakini ukajikuta
unashindwa kudumu naye kwa sababu ya kumuudhi mara kwa mara tena kwa
kusudi, kumnyanyasa, kusikiliza umbea, wivu, kutomjali na kumpuuza.
Kinachosikitisha sana katika mapenzi ni kuona watu wanawapata wapenzi wa
kweli, badala ya kufurahika nao wanawachezea kwa kufanya vurugu na
kuwa waanzilishi wa usaliti na ujeuri. Ushauri wangu ni kuwa, ukipata wa
kukupenda usimchezee, mtunze na umuonyeshe kweli kuwa wewe ni wa
kufanana naye.
Mwisho, mapenzi lazima yakose sababu, ukiulizwa
unampendea nini mpenzi wako? Jibu liwe sijui, kwani ukitaja sababu
yoyote unakuwa katika hatari ya kuachana kwa vile kila sababu ina mwisho
wake. Penzi ni lidhiko la moyo lisilokuwa na kwa nini. Ukisema nampenda
kwa sababu ananijali, asipokujali, ukisema ni mzuri akiwa mbaya, ana
pesa akiishiwa, mtundu uwanjani akichoka? Bila shaka penzi nalo
litachoka!
No comments:
Post a Comment