Friday, 29 May 2015

SIMBA YAFANYA UMAFIA KWA MGOSI,

 

Na Paul Chengula, DAR ES SALAAM

SIMBA SC imemsajili tena mshambuiaji wake wa zamani, Mussa Hassan Mgosi (pichani juu) leo hii, baada ya takriban misimu miwili mizuri akiwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe ameiambia CHENGULA NEWZ, leo mjini Dar es Salaam kwamba wamemrejesha Mgosi kikosini baada ya kuvutiwa na juhudi zake akiwa Mtibwa.
“Kwa Mgosi, Simba ni nyumbani kwake. Alikuwa hapa, tukamuuza DC Motema Pembe (ya DRC), akarudi, akaenda Mtibwa. Na sisi, baada ya kuona bado ana uwezo wa kuisaidia timu yake, tumemrejesha,”amesema Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Mgosi alisajiliwa na Simba SC mwaka 2005 kutoka Mtibwa Sugar na mwaka 2012 akauzwa DC Motema Pembe ya DRC, ambako alicheza kwa misimu miwili.
Mwaka jana, Mgosi alirejea nyumbani baada ya kumaliza Mkataba wake Kongo na kusaini timu yake ya zamani, Mtibwa- lakini baada ya kung’ara Manungu kwa misimu miwili, amerejeshwa kundini.
Mgosi anakuwa mchezaji wa nne kusajiliwa Simba SC ndani ya wiki moja, baada ya awali klabu hiyo kuwasajili kiungo Peter Mwalyanzi kutoka Mbeya City, mabeki Samih Hajji Nuhu kutoka Azam FC na Mohammed Fakhi kutoka JKT Ruvu.
Bahati nzuri ilioyoje kwa Wekundu wa Msimbazi, kama ilivyokuwa kwa Mwalyanzi, Nuhu na Fakhi- Mgosi pia anarejea Simba SC kama mchezaji huru baada ya kumaliza Mkataba wake Manungu. 

No comments:

Post a Comment