KAMATI
ya Usajili ya Simba inaongozwa na wakongwe kabisa katika masuala ya mpira.
Mwenyekiti ni Zacharia Hans Poppe na makamu wake Kassim Mohammed Dewji.
Wawili
hao wamechanganyiwa vijana ambao nao wana damu changa na wana nafasi ya
kuendelea kufanya mambo ya usajili kwa ufasaha kabisa.
Ukiachana
na hivyo, kamati hiyo, bado inaweza kufanya vizuri kwa msaada wa kocha. Iwe ni
ripoti ya Goran Kopunovic ambayo aliiacha, au kocha mpya atakayekuja.
Kwa
kutumia wakongwe hao na vijana ndani ya kamati, pia ujuzi wa kocha, hii ni
nafasi nzuri sana kwa Simba kupata kikosi bora zaidi.
Maoni,
ni jambo jema katika kila jambo la watu. Iwe Dewji au Hans Poppe, au vijana wao
wanaweza pia kupokea maoni na kuyafanyia kazi na mwisho wao ndiyo wenye uwezo
wa kuangalia yapi ni sahihi na yapi si sahihi.
Wao
ndiyo watafanya kazi ya kuchuja na mwisho watapata vitu ambavyo ni sahihi na
kuyafanyia kazi, lakini si kila mwenye nafasi ya uongozi Simba anataka kufanya
usajili.
Usajili
wa Simba una vurugu kubwa. Hili limetokea kwa misimu mitatu sasa. Misimu miwili
wakati wa uongozi wa Ismail Aden Rage na msimu mmoja ndani ya uongozi wa Evans
Aveva
Misimu
miwili ya Rage, usajili wa Simba ulikuwa hovyohovyo, kila mtu alipeleka mtu
wake. Kila mmoja aliona anajua zaidi ya kocha ilimradi mtu wake asajiliwe.
Mwisho
ikafikia viongozi wakaanza kugombea wakitokea kwenye picha ili mradi waonekane
wameshiriki kumsajili mchezaji fulani hivi. Kitu ambacho kilikuwa upuuzi tu,
maana mwisho wake Simba haikufanya lolote licha ya rundo la wachezaji
waliosajiliwa.
Baada
ya misimu hiyo miwili, chini ya uongozi wa Aveva, ikaonekana mambo yatabadilika
kwa kuwa watu wengi walio kwenye uongozi ni wale waliokuwa wakijua kusajili,
kwamba kama wakimtaka fowadi mkali kama Saleh Ally, basi lazima watampata.
Ajabu!
Wao nao wakawa walewale, usajili sasa ukawa haueleweki unafanywa na nani.
Badala ya kamati ya usajili kufanya kazi yake, ikaonekana suala la usajili
limekuwa la kamati ya utendaji ambayo ina watu wengi mno.
Kamati
ya mashindano inasajili, kamati ya fedha nayo inasajili, sasa ikawa ili mradi.
Makamu wa Rais naye anasajili, mwenyekiti wa kila kamati naye anafanya usajili.
Dalili
za kuonyesha Simba watachemsha zilijionyesha mapema. Nikaandika makala
kuwakumbusha kwamba wana kila sababu ya kuheshimu uamuzi wa kocha, pia kuipa
nafasi kamati ya usajili ifanye kazi yake na wao ruksa kupeleka maoni yao.
Nawajua
walioponda, wakiamini kuiachia kamati pekee haikuwa sahihi. Wakajiamini
wanaweza kubadili mambo na kusimamia usajili, mwisho tumeona. Simba imepoteza rundo
la fedha kusajili wachezaji watano wa Uganda, mwisho wa msimu imetema wawili na
bado mmoja amebaki “kimungu” tu.
Sasa
ni wakati mwingine tena ambao Simba inaanza usajili. Viongozi ambao hawahusiki
na usajili wangepunguza kiherehere, halafu wawape nafasi kamati ya usajili
wafanye kazi yao.
Sehemu
ambayo wanaamini wanaweza kuwapa maoni basi wanaweza kufanya hivyo na kuwaachia
wafanye kazi yao.
Kuendelea
kulazimisha wachezaji fulani wasajiliwe kwa kuwa ni watoto wa wajomba zenu,
watu ambao wanawaheshimu sana au mnataka kulipa fadhila kwa kuwa ni watoto wa
michepuko yenu, si sahihi, mnaiumiza Simba na mashabiki wake.
Lazima
mjue mashabiki na wanachama wa Simba, wameumia sana. Huu ndiyo wakati mwafaka
kwa uongozi wenu kurudisha imani kwao kwamba umefika wakati wao pia kubadilika.
Acheni longolongo, wapeni wenzenu wafanye kazi yao na kama mna mawazo,
wafikishieni si kujidai kila mtu anajua na hili ndiyo jambo linaloikwamisha
Simba, mnaamini mnajua sana wakati wengine hamna lolote.
No comments:
Post a Comment