Thursday, 23 July 2015

YANGA SC YATOA NENO JUU YA KMKM HAPO KESHO,SOMA HAPA

Na  Paul  Chengula

YANGA SC itahitaji kuifunga KMKM ya Zanzibar kesho, tena ushindi mzuri ili kujihakikishia nafasi ya Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, michuano inayoendelea Dar es Salaam.
Na KMKM itahitaji ushindi ili pia kujihakikishia kwenda Robo Fainali ya michuano hiyo kutoka Kundi A.
Timu tatu kati ya tano za kundi hilo zitakwenda Robo Fainali kuungana na washindi wawili wa kila kundi B na C pamoja na mshindi wa tatu bora kutoka makundi hayo.
KMKM na Yanga SC kila moja ina pointi tatu baada ya kila timu kushinda mechi moja hadi sasa, dhidi ya wapinzani wale wale, Telecom ya Djibouti.

KMKM imekwishapoteza mechi mbili baada ya kufungwa 2-1 na Khartoum N na 3-1 na Gor Mahia, wakati Yanga SC imepoteza mechi moja tu dhidi ya Gor.
Kama KMKM itafungwa na Yanga SC kesho, ina maana wakitoka Uwanja wa Taifa, watakwenda moja kwa moja kwenye boti za Azam Marine kurejea Zanzibar.
Kocha Ally Bushiri wa KMKM alisema jana bada ya kipigo cha Khartoum kwamba watarudi Uwanja wa Taifa, Ijumaa kupigania ushindi ili kuangalia uwezekano wa kwenda Robo Fainali.
Yanga SC ina mechi nyingine ngumu dhidi ya vinara wa kundi hilo, Khartoum N ya Sudan ambayo itakuwa ya mwisho baada ya kucheza na KMKM kesho.
Gor Mahia walio nafasi ya pili wana ponti sita, mabao matano ya kufunga na mawili ya kufungwa.Khartoum ina pointi sita, mabao saba ya kufunga na moja la kufungwa, wakati
Yanga SC inashika nafasi ya tatu kwa pointi zake tatu, mabao manne ya kufunga na mawili ya kufungwa, wakati KMKM ina pointi tatu, mabao matatu ya kufunga na matano ya kufungwa.
Telecom ya Djibouti ambayo itacheza mechi ya mwisho na Gor Mahia kabla ya kuelekea Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kupanda ndege ya kurejea Djibouti haijashinda mchezo hata mmoja hadi sasa baada ya kufungwa mechi zote tatu.
Ilifungwa 1-0 na KMKM, ikafungwa 5-0 na Khartoum na jana imefungwa 3-0 na Yanga SC. 
Hadi sasa unaweza kusema Khartoum na Gor Mahia tayari zipo Robo Fainali, lakini nafasi ya tatu inagombewa na Yanga SC na KMKM-maana yake mechi ya kesho ni ya ‘kukata na shoka’.
Na kihistoria timu za Zanzibar zinapokutana na vigogo wa Bara katika michuano hii ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) huwa ni ‘patashika nguo kuchanika’ basi Yanga kazi wanayo kesho. 

No comments:

Post a Comment