Friday 11 December 2015

SIMBA FITI KUIVAA AZAM,WENYEWE WATOA NENO



Na PAUL CHENGULA, DAR ES SALAAM
 
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inarejea kesho baada ya mapumziko ya takriban mwezi mzima kupisha mechi za timu ya taifa na michuano ya Kombe la CECAFA Challenge.
Nyasi za viwanja sita zitawaka moto kesho, lakini macho na masikio ya wengi vitaelekezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako vigogo Simba SC watakuwa wanamenyana na Azam FC.
Azam FC wanahitaji ushindi katika mchezo wa kesho kujiimarisha kileleni na kuzidi kuwaacha mabingwa watetezi, Yanga SC wakati Simba SC inahitaji ushindi ili kurudi kwenye mbio za ubingwa.
Na hapo ndipo ulipolalia utamu na msisimko wa mchezo huo, kiasi kwamba hata mashabiki wa Yanga ingawa timu yao itakuwa Uwanja wa Mkwakwani kesho ikimenyana na Mgambo JKT, lakini watakuwa wanasikilizia kinachoendelea Taifa.
Na sana Yanga SC wanaitakia ushindi Simba SC au hata sare, ili mahasimu wao hao, Azam FC katika mbio za ubingwa wapunguzwe kasi. 
Simba SC imeimarisha kikosi chake katika dirisha dogo kwa kumrejesha mshambuliaji wake Mkenya, Paul Kiongera aliyekuwa anacheza kwa mkopo KCB ya kwao.
Aidha, Wekundu hao wa Msimbazi pia wamesajili chipukizi wawili, beki wa kati Novat Makunga kutoka African Sports ya Tanga na mshambuliaji Hajji Ugando kutoka Mtibwa Sugar B, ingawa haijulikani kama watakamilishiwa utaratibu wa kupata leseni kabla ya mechi za kesho.
Azam FC yenyewe imemsajili kipa mkongwe, Ivo Mapunda aliyewahi kudakia Yanga SC, Tukuyu Stars, Prisons, Moro United, African Loyon, Simba za Tanzania pia na St George ya Ethiopia na Gor Mahia ya Kenya.
Mabingwa watetezi, Yanga SC wao kesho watakuwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kumenyana na timu ngumu, MGambo JKT ya Kabuku, Tanga.  
Mechi nyingine za ligi hiyo kesho; Kagera Sugar wataikaribisha Ndanda FC Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, Stand United wakiongozwa na kinara wa mabao Ligi Kuu, Elias Maguri wataikaribisha Mwadui FC, Mbeya City wataikaribisha Mtibwa Sugar, Majimaji wataikaribisha Toto Africans, wakati Jumapili JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Karume na Coastal Union watamenyana na mahasimu wao, African Sports.

No comments:

Post a Comment